Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNICEF yafikia karibu watoto nusu ya dunia na chanjo

UNICEF yafikia karibu watoto nusu ya dunia na chanjo

Watoto karibu nusu ya dunia wenye umri wa chini ya miaka mitano wamefikiwa na dozi bilioni 2.5 za chanjo zilizotolewa na shirika la Umoja wa mataifa la kuhudumia watoto UNICEF mwaka 2016.

Takwimu zilizotolewa katika wiki ya chanjo duniani zinalifanya shirika hilo kuwa ndio mnunuzi mkubwa wa chanjo kwa ajili ya watoto duniani. Nchi tatu ambazo bado zinasumbuliwa na polio duniani ndizo zilizopokea asilimia kubwa ya chanjo hizo kuliko nchi nyingine zozote, Nigeria ikipata dozi milioni 450, Pakistan milioni 359 na Afghanistan zaidi ya dozi milioni 150.

UNICEF inasema fursa ya upatikanaji wa chanjo imepunguza vifo vya watoto wa chini ya miaka mitano vitokanavyo na surua,kuhara, homa ya vichomi vikali na pepopunda kwa kiasi kikubwa kuanzia 2000 hadi 2015.

Hata hivyo shirika hilo linasema bado kuna watoto zaidi ya milioni 19 kote duniani hawapati chanjo kila mwaka huku watoto zaidi ya milioni moja wakipoteza maisha kwa magonjwa yanayozuilika kwa chanjo na vifo vingi hutokea katika nchi masikini.