Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Afghanistan imepiga hatua mapambano dhidi ya rushwa: UM

Afghanistan imepiga hatua mapambano dhidi ya rushwa: UM

Umoja wa Mataifa umekaribisha mafanikio ya mapambano dhidi ya rushwa nchini Afghanistan na kusema licha ya changamoto kadhaa zinazosalia katika taifa hilo linalokabiliwa na mchafuko, lazima rushwa itokomezwe.

Akinukuliwa katika ripoti iliyotolewa leo Jumanne, Tadamichi Yamamoto, ambaye ni Mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu nchini Afghanistan, amesema Umoja wa Mataifa unaunga mkono juhudi za serikali za kukabiliana na rushwa na kukomesha ukwepaji wa sheria.

Amesema hatua hiyo pia itahakikisha uwajibikaji, uwazi na kuhifadhi uadilifu katika usimamizi wa huduma za umma, fedha na mali asili.

Ripoti hiyo iliyopewa jina Mapambano ya Afghanistan dhidi ya Rushwa: Uwanja mwingine wa mapambano,ambapo ilisambazwa na ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini humo UNAMA, kwa wizara na mahakama za Afghanistan kabla ya kuitoa, inaeleza jinsi gani rushwa imeathiri nyanja zote za maisha katika taifa hilo na kushusa imani ya umma kwa taasisi za serikali pamoja na kukwamisha juhudi za kurejesha amani ya kudumu na mafanikio nchini humo.