Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Suluhu pekee ya machafuko Sudan kusini ni muafaka wa kisiasa

Suluhu pekee ya machafuko Sudan kusini ni muafaka wa kisiasa

Baraza la Uslama la Umoja wa Mataifa Jumanne limekuwa na kikao kupata taarifa kuhusu mpango wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan kusini UNMISS na vikwazo dhidi ya taifa hilo changa. Akitoa taarifa kwenye kikao hicho mwakilishi maalumu wa Umoja wa Mataifa Sudan Kusini na mkuu wa UNMISS David Shearer amesema hakuna sehemu ya taifa hilo iliyo na kinga dhidi ya machafuko, na pia hakuna juhudi za msingi zilizofanywa na pande zote katika mzozo kuhakikisha usitishaji uhasama, badala yake nchi hiyo imeendelea kushuhudia ongezeko la machafuko hususani mwezi uliopita.

Amesema machafuko mengi yanachochewa na kila upande kutaka kunyakua maeneo yanayodhibitiwa na upinzani kabla ya msimu wa masika kuanza hivyo Umoja wa Mataifa umeimarisha ulinzi.

(Sauti ya Shearer)

"Katika taswira ya machafuko hayo katika miezi iliyopita, UNMISS imeimarisha ulinzi wake. Doria yetu jumuishi kwa maeneo mengi yenye misukosuko imeongezeka, kwa lengo la kuzuia vurugu, kufuatilia na kutoa taarifa kuhusu hali ya haki za binadamu, na pia kujihusisha kisiasa na vyama katika ngazi za chini. "

Bwana Shearer amesisitiza kuwa suluhu ya kisiasa pekee ndio itamaliza adha Sudan kusini

(Sauti ya Shearer )

“Licha ya kinachoonekana kuwa jaribio la pande zote kutaka ushindi kupitia mtutu, suluhu ya kisiasa ndio njia pekee ya kusonga mbele kwa Sudan kusini. Lakusikitisha ni kwamba hakuna upande ulioonyesha nia ya kufufua mkataba wa amani.”

Hata hivyo amesisitiza kwamba mchakato wa kisiasa haujafa nchini humo bali unahitaji kufufuliwa upya na amesema UNMISS itashirikiana na wadau katika kusaka fursa za kupata suluhu itakayomaliza vita na madhila kwa watu wa Sudan kusini.