Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Changamoto ya kumaliza mizozo ni kuwekeza katika kuizuia-Guterres

Changamoto ya kumaliza mizozo ni kuwekeza katika kuizuia-Guterres

Changamoto kubwa ya kukomesha mizozo na vita ni kuwekeza katika kuzuia migogoro hiyo isitokee. Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres Ijumaa akizungumza katika ufunguzi wa mkutano kuhusu ufadhili kwa ajili ya amani:ubunifu wa kukabiliana na hali tete unaofanyika mjini Washington D.C hapa Marekani.

Mkutano huo unaohusisha wadau mbalimbali ikiwemo pia benki ya dunia na shirika la fedha duniani IMF unajikita katika ajenda ya amani endelevu na ufadhili kwa waathirika wa mizozo. Guterres amesema migogoro ni mingi sana duniani kuanziaa Somalia hadi Syria na kuathiri mamilioni ya watu.

(SAUTI YA GUTERRES)

“Tunashuhudia ongezeko la migogoro mipya na migogoro ya zamani ikiendelea na yote inahusiana na kitu kimoja, hali tete, hali tete ya nchi, hali tete ya taasisi na hali tete ya jamii, ambavyo vinachagiza mizozo na kufanya kuwa vigumu kuipatia suluhu na kuondokana nayo.”

Ameongeza kuwa ingawa juhudi nyingi zinafanyika ikiwemo kuwasaidia mamilioni ya waathirika changamoto kubwa ni

(SAUTI YA GUTERRES)

“Kikubwa kwangu ni jinsi gani tunaweza kuishawishi jumuiya ya kimataifa kwamba uwekezaji muhimu na wa lazima ni kuwekeza katika kuzuia na kushughulikia hali tete kabla hatujachelewa. Maana yake ni kuimarisha nchi, kuimarisha taasisi, kuboresha asasi za kiraia, kujumuisha mtazamo wa amani na usalama, ujumuishi endelevu na mtazamo wa haki za binadamu”

Amesisitiza kuwa endapo haya yatafanikiwa basi migogoro mingi mipya itaweza kuzuiliwa na ya zamani kupatiwa suluhu.