Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UM kupunguza gharama katika shughuli zake mashinani-Gutteres

UM kupunguza gharama katika shughuli zake mashinani-Gutteres

[caption id="attachment_315977" align="aligncenter" width="625"]matumiziguterres

Kama sehemu ya tathimini inayoendelea ya Umoja wa Mataifa kuhusu gharama na matumizi ya rasilimali zinazotolewa na nchi wanachama, leo Alhamisi Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amezindua mradi wa kupunguza gharama kwa kuongeza ufanisi wa rasilimali zake za anga.

Kupitia taarifa iliyotolewa na msemaji wake Alhamisi Umoja wa Mataifa umesema hivi sasa una ndege za kudumu 58 na zinazozunguka kwa awamu 157, Katika operesheni 12 za ulinzi wa amani na operesheni 6 za kisiasa. Kwa kipindi cha 2015-2016 gharama za uendesheaji wa ndege hizo kwa mwaka inakaribia dola milioni 750.

Wakati rasilimali hizo zinatoa msaada muhimu wa kiufundi na uwezeshaji wa kijeshi , kutokana na gharama, Katibu Mkuu amewaomba wakuu wa vitengo husika vya operesheni za Umoja wa Mataifa mashinani kutathimini na kufanya mabadiliko ya matumizi yake kwa kutafuta suluhu mbadala ambayo gharama zake zitakuwa nafuu. Ameongeza kuwa hii pia ni fursa ya mipango hiyo ya operesheni za Umoja wa mataifa kuwa wabunifu.

Wakati tathimini ikiendelea Katibu Mkuu ametoa ombi la kuhakikisha safari za abiria zinapunguzwa na kufanyika zile tu ambazo ni za muhimu na mipango iwe ni ile ya kupunguza safari na safari maalumu ziwe za nadra.

Guterres ameongeza kuwa sekretarieti ya Umoja wa Mataifa inabeba mzigo wa uwajibukaji linapokuja suala la matumizi ya fedha na rasilimali zinazotolewa na nchi wanachama. Ameiomba idara inayohusika na msaada mashinani kuongoza na kuratibu mradi huu kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa.