Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ukaguzi baada ya zahma ya 2016 Juba umefanyika

Ukaguzi baada ya zahma ya 2016 Juba umefanyika

Ukaguzi mwingine ulioongozwa na Meja Jenerali mstaafu Patrick Cammaert umefanyika mwezi Machi nchini Sudan Kusini, kufuatia ripoti ya uchunguzi uliobainisha kuwa Ujumbe wa Umoja Mataifa nchini humo, UNMISS haukuwajibika ipasavyo katika ulinzi wa raia Julai 2016.

Matokeo ya ukaguzi huo yaliyowasililishwa mbele ya Rais wa Baraza la Usalama na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres yanasema, yamebaini mabadiliko chanya baada ya UNMISS kutekeleza mapendekezo yaliyotolewa katika ripoti ya uchunguzi wa awali uliobaini kuwa ujumbe huo ulishindwa kuzuia ghasia zilizosababisha vifo vya raia 73 wakiwemo wakimbizi wa ndani.

Kwa mujibu wa msemaji wa UNMISS, Daniel Dickinson, mabadiliko hayo ni pamoja na uimarishwaji wa ulinzi wa raia na jinsi ya kukabiliana na migogoro katika kambi ya ulinzi wa raia sanjari na mamlaka iliyopewa, na kikubwa zaidi..

(Sauti ya Daniel)

"Ni kupiga marufuku silaha katika kambi ya ulinzi wa raia na jengo la Umoja wa Mataifa Juba, ambayo imepunguza kwa kiasi kikubwa migogoro pamoja na visa vya ukatili wa kingono na kijinsia."