Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UM na AU wasaini mkakati mpya wa amani na usalama-Guterres

UM na AU wasaini mkakati mpya wa amani na usalama-Guterres

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amesema mkutano wa kwanza baina yake na mwenyekiti wa tume ya muungano wa Afrika Moussa Faki Mahamat unawakilisha historia na ishara njema ya kuboresha ushirika baina ya mashirika hayo mawili katika nyanja mbalimbali za masuala ya amani, ulinzi, usalama, maendeleo na vita dhidi ya ugaidi.

Pia amesema mashirika hayo mawili yana mtazamo mmoja kwamba amani na usalama, ujumuishwa na maendeleo endelevu , haki za binadamu na utawala bora ni mambo ambayo yanapaswa kuchukuliwa kwa pamoja , kwa mtazamo mmoja na kuimarisha ushirika wao.

(Sauti ya Guterres)

"Nimefurahi kwamba tumeweza kutia saini mkakati mpya ambao utaimarisha ushirika wwetu katika masuala ya amani na usalama. Ni lazima tufikirie kwamba Afrika kama ilivyo sehemu zingine duniani mabadiliko katika hali ya usalama yanatulazimisha kutathimini upya mikakati yetu ya jinsi operesheni za mani zinavyofanityika.”

Ameongeza kuwa ushirika wao pia utahakikisha kwamba ajenda ya maendeleo ya Afrika ya 2063 inakwenda sanjari na mikakati ya maendeleo endelevu yaani SDG’s.

Kwa upande wake mwenyekiti wa tume ya AU Afrika Moussa Faki Mahamat amesema yaliyopita si ndwele ni wakati wa kuganga yajayo.

(Sauti ya Mahamat)

"Nafikiri muda umefika, kufanya tathimini muhimu ya madhaifu na nguvu na kufanya kazi pamoja kuimarisha operesheni za ulinzi wa amani barani Afrika. Jambo muhimu zaidi ni kuwa pamoja, kufanya kazi, kujadili na kutoa taarifa pamoja. Naamini huu ni ukurasa mpya katika ushirikiano kati ya Umoja wa Mataifa na Muungano wa Afrika."