Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ingawa kuna matumaini, hali bado ni tete Somalia na Sudan Kusini-UM

Ingawa kuna matumaini, hali bado ni tete Somalia na Sudan Kusini-UM

Hali ya kibinadamu nchini Somalia na Sudan Kusini bado ni tete kutokana na vita vinavyoendelea, ukame na maradhi.

Hayo yamesemwa na ujumbe wa Umoja wa Mataifa kutoka shirika la kuratibu masuala ya kibinadamu na misaada ya dharura (OCHA), shirika la idadi ya watu duniani (UNFPA) shirika la mpango wa maendeleo (UNDP) na shirika la kuhudumia watoto (UNICEF) uliozuru nchi hizo mbili kutathimini hali halisi.

Ujumbe huo ukizungumza na waandishi wa habari Jumanne mjini New York umesema hatua zimepigwa na wahudumu wa misaada ya kibinadamu kufikisha huduma na misaada inayohitajika kwa walengwa lakini bado kuna changamoto nyingi. John Ging ni mkurugenzi wa idara ya operesheni OCHA

(SAUTI YA JOHN GING)

image
John Ging ni mkurugenzi wa idara ya operesheni OCHA.(Picha:UM/Manuel Elias)
“Nchi zote Somalia na Sudan Kusini ziko katika hatihati ya baa la njaa na Sudan kusni baa limeshatangazwa, hivyo kuna tatizo kubwa la uhakika wa chakula katika nchi hizi , kwa Somalia watu milioni 6.2 wanahitaji msaada wa kibinadamu na pia kuna tishio la surua , na kilicho bayana ni kwamba masuala ya ulinzi ni changamoto kubwa, Somalia ni hatari kwa watu wake, na ni mazingira magumu kwa wahudumu wa misaada kufanya kazi.Mahitaji yanaongezeka haraka lakini juhudi za msaada zinaenda sanjari na mahitaji hayo kwa sasa.”

Kwa upande wake Ugochi Daniels mkuu wa UNFPA kitengo cha masuala ya kibinadamu katika mazingira magumu amesema wanawake na watoto ndio wanaolipa gharama kubwa katika hali mbaya inayozikabili nchi hizo mbili

(SAUTI YA UGOCHI )

image
Ugochi Daniels mkuu wa UNFPA kitengo cha masuala ya kibinadamu katika mazingira magumu.(Picha:UM/Manuel Elias)
"Kilichonigusa zaidi ni ukweli kwamba taswira ya zahma hii ni mwanamke na mtoto, katika nchi zote hizi mbili kuna zaidi ya wanawake 250,000 wajawazito ambao wameathirika na mzozo. Ndio kuna utapia mlo ,ndio kuna kipindupindu lakini katika hili pia kuna hatari kubwa ya ukatili wa kingono. Sudan Kusini msichana ana nafasi kubwa ya kufariki dunia akijifungua kuliko kumaliza shule, na Somalia mmoja kati ya wanawake 18 wajawazito hufa kutokana na kujifungua au matatizo ya mimba.”

Naye mwakilishi wa UNDP Mburad Wahba amesema amejumuika na ujumbe huo kwenda Somalia na Sudan Kusini kuangalia jinsi gani suala la maendeleo linaweza kuchangia kupunguza makali ya hali ya sasa. Amesema UNDP imekuwa ikijishughulisha kwa kila hali hasa Somalia kuhakikisha mipango ya maendeleo kwa msaada wa wafadhili inapewa kipaumbele.