Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tugeuze SDG's kuwa biashara itakayonufaisha wote

Tugeuze SDG's kuwa biashara itakayonufaisha wote

Mkutano wa ngazi ya juu kuhusu gharama ya kufikia malengo ya maendeleo endelevu, SDG mwaka 2030 umefanyika leo kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa New York, Marekani kuhamasisha ushirikiano baina ya kampuni binafsi na wadau wengine, kutathmini nini hasa kifanyike kupata takriban dola trilioni 6 kila mwaka kufikia malengo hayo.

Kongamano hilo lililopewa jina la "SDG FINANCING LAB" ulihudhuruwa na wadau kadhaa wakiwamo Benki ya Dunia na kampuni binafsi, ambapo Naibu Katibu Mkuu wa umoja huo, Bi. Amina Mohammed akawaeleza umuhimu wa ushirikiano huo akisema..

(Sauti ya Amina)

" Ni kwa maslahi ya nchi zote, kampuni na watu kupenya ndani ya utajiri wa uzuri ambao utaletwa na maendeleo endelevu katika mazingira, uchumi na kwa jamii. Tunahitaji rasilimali muhimu ili kufikia ndoto hii ya kimataifa ya kutomuacha mtu nyuma. Hivyo ni muhimu sana kuchukua mbinu ya kimkakati itakayotumia uwekezaji wote."

image
Rais wa Baraza Kuu Peter Thompson. Picha: UN Photo/Rick Bajornas
Naye Rais wa Baraza Kuu Peter Thompson akatoa wito kwamba bila kufikia malengo haya na kuwekeza katika maisha endelevu ya baadaye, basi mwanadamu yumo hatarini zaidi, na hivyo ushiriki wa sekta binafsi ndio ufunguo wa kuhamasisha mitaji itakayogeuza SDG kutoka ndoto na kuwa hali halisi.

(Sauti ya Thompson)

"Uendelevu unazidi kujulikana ulimwenguni kote kama mantiki thabiti na ya kibiashara. Na changamoto mbele yetu ni kuongeza juhudi zaidi ili kuhamasisha rasilimali na kuongeza zaidi mpito wa uchumi kuwa mifano jumuishi na endelevu. Kemia ya mafanikio yatasalia katika milinganyo ya mantiki hiyo, pamoja na kufikia changamoto hiyo."