Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Pande kinzani Sudan Kusini zatakiwa kuweka maslahi ya raia mbele

Pande kinzani Sudan Kusini zatakiwa kuweka maslahi ya raia mbele

Pande kinzani katika mzozo wa Sudan Kusini zimetakiwa na maafisa wa ngazi ya juu wa Umoja wa mataifa nchini humo, kuweka maslahi ya raia mbele kwa kujizuia katika wakati huu wa machafuko na kukumbuka wajibu wao katika kulinda raia kwenye vita hivyo.

Kumezuka mapigano mapya baina ya serikali na majeshi ya upinzani katika maeneo mbalimbali nchini humo ikiwemo mji wa Raga Magharibi wa Sudan Kusini, Waat Jonglei Mashariki na maeneo ya Wunkur na Tonga Kaskazini mwa jimbo la Upper Nile.

Mapigano hayo yanafuatia yale yaliyozuka hivi karibuni mjini Pajok na ya wiki moja iliyopita ya mjini Wau na viunga vyake yaliyosababisha vifo na maelfu ya watu kufungasha virago.