Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kipindupindu na Kuhara vyaua zaidi ya watu 500 Somalia

Kipindupindu na Kuhara vyaua zaidi ya watu 500 Somalia

Watu zaidi ya 500 wamefariki dunia nchini Somalia kutokana na ugonjwa wa kuhara na kipindupindu tangu mwanzoni mwa mwaka huu. Assumpta Massoi na ripoti kamili.

(Taarifa ya Assumpta)

Ukame nchini Somalia unahatarisha uhai wa wananchi hasa katika masuala ya kujisafi na kupata maji safi na salama, ambapo ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya kibinadamu, OCHA imesema vifo hivyo ni kati ya watu zaidi ya 21,000, waliokumbwa na ugonjwa huo.

OCHA inasema kuwa uwiano wa ugonjwa na kifo ni asilimia 2.1, kiwango ambacho ni kikubwa na kinaonyesha hatari zaidi iwapo hatua hazitachukuliwa, maeneo yaliyoathirika zaidi yakitajwa kuwa ni Juba Kati na Bakool.

Wakati ukame ukisababisha uhaba waji na vifo, shirika la mpango wa maendeleo la Umoja wa Mataifa, UNDP limesema mafanikio ya miaka mitano ya ujenzi wa Somalia yako hatarini kutoweka kutokana na janga la sasa.

David Akopyan ni mkurugenzi mkazi wa UNDP, Somalia.

(Sauti ya David)

“Bila shaka, katika janga la sasa hatua muhimu kuchukua ni kuimarisha usaidizi wa kibinadamu na kufanya kadri iwezekanavyo kuokoa maisha, lakini wakati huo huo tunafahamu kuwa iwapo ukame ukileta njaa kali kama ilivyokuwa mwaka 2011, sanjari na matatizo ya kibinadamu na njaa kali kwa watu wengi, basi itatokomeza miradi yote ya ujenzi wa nchi na mafanikio yote yaliyopatikana.”