Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Urusi yapinga azimio la kuwajibisha Syria

Urusi yapinga azimio la kuwajibisha Syria

Matumaini ya kupitishwa kwa rasimu ya azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa dhidi ya shambulio linaloelezwa kuwa la kemikali huko Syria wiki iliyopita, yametoweka baada ya Urusi ambayo ni mjumbe wa kudumu wa baraza hilo kupinga kwa kutumia kura turufu.

Rasimu hiyo iliandaliwa na Uingereza na kujadiliwa miongoni mwa nchi tatu zenye ujumbe wa kudumu kwenye baraza hilo ambazo ni Uingereza, Marekani na Ufaransa.

Lengo la rasimu hiyo pamoja na kulaumu shambulio hilo, pia ililenga kuitaka Syria ishirikiane kikamilifu na wachunguzi wa shirika la Umoja wa Mataifa la kupinga silaha za kikemikali, OPCW.

Hata hivyo baada ya rais wa Baraza hilo kwa mwezi huu wa Aprili, Balozi Nikki Hailey wa Marekani kuwasilisha mezani lipigiwe kura na wajumbe 15, matokeo yakawa kama ifuatavyo..

(Nats.)

image
Balozi wa Urusi kwenye Umoja wa mataifa Vladmir Safrokov akihutubia baraza la usalama ya kujadili matumizi ya silaha za kemikali kwenye mji wa Khan Shaykhun nchini Syria Picha: UM/-Evan Schneider
Balozi Nikki anasema kuwa kura 10 zimesema ndiyo, kura mbili hapana na wajumbe watatu hawakupiga kura kabisa. Hivyo azimio halijapita kwa kuwa mwanachama wa kudumu amepinga kwa kutumia kura turufu.

Nchi ambazo hazikupiga kura kabisa ni China, Ethiopia na Kazakhstan, huku Bolivia ikiungana na Urusi kupinga.

Akieleza sababu za kupinga, mwakilishi wa kudumu wa Urusi kwenye Umoja wa Mataifa balozi Vladmir Safroko amesema hakukuwepo na uhraka wa kuwasilisha azimio hilo kwa kuzingatia kuwa kesho OPCW itakuwa na kikao cha kujadili suala hilo la silaha za kemikali Syria,  na zaidi ya yote...

(Sauti ya balozi Safroko)

 “Iwapo wenzetu wanaamini ni muhimu kupitisha azimio dhidi ya silaha kemikali nchini Syria, tuanze kushirikiana na kuandaa nyaraka moja ambayo nasi tutaweka mitazamo yetu inayoungwa mkono na taarifa za juu ya silaha za kemikali zinazotumiwa na magaidi.”

Naye Balozi Nikki akizungumza kwa niaba ya nchi yake Marekani akasema kuwa..

(Sauti ya balozi Nikki)

“Kwa kutumia kura yake turufu, Urusi imekataa uwajibikaji, Urusi imekataa ushirikiano na  jopo huru la uchunguzi la Umoja wa Mataifa Urusi imekataa azimio ambalo lingesaidia kuchagiza amani Syria.”

image
Balozi wa Marekani kwenye umoja wa Mataifa ambaye pia ni Rais wa baraza la usalama mwezi huu Nikki Haley akihutubia baraza la usalama. Picha: UN Photo/Rick Bajornas
Wajumbe ambao hawakuonyesha msimamo wowote wakihutubia wamesema kuwa wanaamini kuwa hakuna mtu anayetetea matumizi ya silaha za kemikali, lakini wanaamini kuwa kama mashauriano yangalifanyika kwa kina, baadhi ya vipengele vinavyoleta ukinzani vingalipatiwa ufumbuzi.

Mwakilishi wa  Syria kwenye Umoja wa Mataifa, balozi Bashar Ja'afari akaeleza kile ambacho wamefanya kufanikisha uchunguzi...

(Sauti ya Balozi Ja’afari)

“Nchi yangu katika misingi ya kuendeleza uwazi na ushirikiano na OPCW ikimtaka atume jopo huru, lenye haki na lenye ueledi litakalokwenda huko Khan Sheikhoun na kituo cha kijeshi cha Shayrat. Kwa bahati mbaya huko Khan Sheikhoun, kibali lazima kitolewe na magaidi wa Jabhat Al Nusra na wengineo wanaoshikilia eneo hilo.”

image
Mapema asubuhi, mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kwa Syria Staffan de Mistura alihutubia baraza hilo la usalama na kueleza kuwa hali nchini humo ni mbaya na sasa ni wakati wa chombo hicho kusaidia mchakato wa mazungumzo ya kumaliza vita vilivyodumu miaka sita sasa.

Amesema mchakato huo wa mazungumzo kati ya serikali na upinzani nchini Syria hivi sasa ni tete na uko hatarini.