Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto waendelea kutumiwa na Boko haram – UNICEF

Watoto waendelea kutumiwa na Boko haram – UNICEF

Idadi ya watoto wanaotumiwa na magaidi wa Boko Haram kwenye mashambulizi katika mzozo unaoendelea huko bonde la ziwa Chad imevunja rekodi katika robo ya kwanza ya mwaka huu.

(Taarifa ya Assumpta)

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF limesema kupitia ripoti yake iliyotolewa kuwa katika kipindi hicho watoto 27 walitumiwa kubeba mabomu na kulipua huko Nigeria, Chad, Niger na Cameroon, idadi ambayo ni sawa na ile ya mwaka mzima wa 2016.

Mkurugenzi wa UNICEF ukanda wa Afrika Magharibi na Kati Marie-Pierre Poirier amesema ongezeko hilo linaonyesha mbinu mpya ya magaidi hao ambapo watoto hao ni pamoja na wa kike.

Femi ni mmoja wa wavulana waliowahi kutekwa na Boko Haram na sasa yuko huru na anasimulia masahibu yao..

(Sauti ya Femi)

“Tuko wengi sana ambao tulitekwa. Walikuwa wanatupiga kila siku. Baadhi ya mambo ambayo wanatufundisha ni mabaya. Watakufundisha hata kuua.”

Kutokana na vitendo kama hivi, Mkurugenzi huyo wa UNICEF amesema watoto hao hawana nia ya kutekeleza ukatili huo bali wanalaghaiwa, jambo ambalo amesema ni la aibu.