Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Utekelezaji wa adhabu ya kifo waendelea kupungua- Amnesty

Utekelezaji wa adhabu ya kifo waendelea kupungua- Amnesty

Ripoti mpya ya shirika la kimataifa la kutetea haki za wafungwa, Amnesty International imeonyesha kuwa idadi ya watu duniani ambao walihukumiwa adhabu ya kifo mwaka jana ilikuwa 3,117, kiwango ambacho amesema ni pungufu kwa asilimia 37 ikilinganishwa na mwaka uliotangulia wa 2015.

Akiwasilisha ripoti hiyo leo kwenye makao makuu yaUmoja wa Mataifa jijini New York, Marekani, mwakilishi wa shirika hilo kwenye umoja huo Renzo Pomi amesema kati ya hao waliohukumiwa, walionyongwa ni 1,032.

Amesema alisema asilimia 83 ya adhabu hiyo ilitekelezwa katika nchi za Iran, Saudi Arabia, Iraq na Pakistani.

Bwana Pomi ametaja sababu ya kupungua kwa adhabu ya kifo kuwa ni nchi 104 kuondokana na adhabu hiyo mwaka jana ilihali 144 tayari zimepitisha sheria za kuachana nayo kabisa.

Halikadhalika amesema ripoti hiyo imeonyesha China imeendelea kushika namba moja katika kutekeleza adhabu ya kifo ambapo ingawa takwimu zake kamilifu za utekelezaji wa adhabu hiyo zinasalia kuwa siri kubwa.

Umoja wa Mataifa unapigia chepuo kupigwa marufuku kwa adhabu ya kifo ukisema kuwa ni kinyume na haki za binadamu.