Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hatukubali migahawa Somalia kugeuka maeneo ya umwagaji damu- Keating

Hatukubali migahawa Somalia kugeuka maeneo ya umwagaji damu- Keating

Mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia, Michael Keating amelaani vikali mwendelezo wa hivi karibuni wa matukio ya kigaidi ambayo yamesababisha vifo na majeruhi miongoni mwa wananchi.

Mathalani katika siku 10 zilizopita, mashambulizi zaidi ya kumi yanayodaiwa kufanywa na Al Shabaab yamesababisha vifo vya raia 28 na majeruhi 31.

Taarifa ya ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia, UNSOM imemnukuu Keating akisema kuwa mashambulizi hayo yalitekelezwa kwenye maeneo ya raia na hivyo kugeuza migahawa, masoko na mabasi ya abiria kuwa maeneo ya umwagaji damu na machungu.

Keating ambaye pia ni mkuu wa UNSOM amesema mashambulizi dhidi ya raia hayawezi kuhalalishwa kwa misingi yoyote ile na ni kinyume na ubinadamu kutumkia hatua hiyo kusongesha maslahi ya kisiasa.

Ametuma rambirambi kwa wafiwa na kuwatakia ahueni majeruhi.