Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Biashara huria imekuwa mwiba kwa wengi- Ripoti

Biashara huria imekuwa mwiba kwa wengi- Ripoti

Ripoti mpya ya mashirika matatu ya Umoja wa Mataifa kuhusu jinsi ya kufanya biashara iwe injini ya ukuaji kwa wote, imesema manufaa ya biashara huria ulimwenguni yameambatana machungu katika baadhi ya maeneo dunia.

Ikizinduliwa hii leo huko Ujerumani, ripoti hiyo iliyoandaliwa na Benki ya Dunia, shirika la fedha duniani, IMF na lile la biashara WTO limesema pamoja na kufungua milango kwa walaji kuwa na fursa nyingi za kuchagua, ushindani umekuwa mwiba kwa baadhi ya nchi.

Imesema suluhu si sera pekee bali pia sera zinazotambua changamoto zitokanazo na biashara huria ikiwemo kubadilika kwa mwelekeo wa ajira, teknolojia na ubunifu.

Kwa mantiki hiyo serikali zinapaswa kuweka mazingira bora ya sera za ajira ikiwemo mafunzo kwa wafanyakazi, usaidizi kwenye kusaka ajira ili kuweza kujumuisha wafanyakazi ambao wanapoteza ajira kutokana na mabadiliko ya mazingira ya kazi.

Akifafanua hoja hiyo, mkurugenzi mkuu wa WHO Roberto Azevêdo amesema changamoto iliyopo sasa ni kusaidia wafanyakazi wa leo na kuwapatia mafunzo wafanyakazi wa kesho ili kuhakikisha kuwa mfumo wa sasa wa biashara unakuwa jumuishi.