Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mashirika ya UM yasaidia kampeni dhidi ya Polio, Yemen

Mashirika ya UM yasaidia kampeni dhidi ya Polio, Yemen

Takribani watoto milioni tano nchini Yemen wamepatiwa chanjo dhidi ya ugonjwa wa Polio, katika nchi hiyo ambayo iko katikati ya vita kwa miaka miwili sasa.

Kampeni hiyo ya kitaifa imefanikishwa kufuatia ushirikiano baina ya mashirika ya Umoja wa Mataifa likiwemo lile la kuhudumia watoto, UNICEF, lile la afya, WHO na Benki ya Dunia.

Ikiwa imezinduliwa mwezi Februari mwaka huu, kampeni ililenga watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano kwenye majimbo yote ya Yemen ambapo imetajwa kuwa katika jimbo la Sa’ada watoto 369,000 wenye umri wa kati ya miaka sita hadi 15 walipatiwa chanjo dhidi ya Surua.

WHO imesema kabla ya mwaka 2006, ugonjwa wa Polio ulikuwa unaongoza kwa kusababisha vifo miongoni mwa watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano lakini hivi sasa viwango vimepungua kutokana na kampeni kadhaa zinazofadhiliwa na mashirika hayo matatu.

Vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini vimesambaratisha mifumo ya afya ikiwemo mipango ya utoaji chanjo za kinga dhidi ya magonjwa kwa watoto.