Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nusu ya familia Iraq wakabiliwa na uhaba wa chakula: WFP

Nusu ya familia Iraq wakabiliwa na uhaba wa chakula: WFP

Zaidi ya nusu ya familia nchini Iraq ziko katika hatari ya ukosefu wa chakula na haziwezi kuendelea kuhimili majanga kama vile machafuko na kuongezeka kwa bei ya chakula, imesema ripoti ya shirika la mpanmgo wa chakula duniani, WFP na serikali ya Iraq.

Ripoti hiyo iliyoangazia kwa kina ukosefu wa chakula nchini Iraq, inaonya kuhusu kiwango kikubwa cha hatari hasa utapiamlo kwa watoto na ustawi wa jamii wakati huu ambapo zaidi ya nusu ya kaya nchini humo hazina uhakika wa chakula.

Dina El-Kassaby, afisa wa WFP anaelezea baadhi ya mapendekezo yaliyomo kwenye ripoti hiyo.

(Sauti ya Dina)

“Kuboresha uelewa wa lishe, kuimarisha fursa ya elimu kwa watoto wa kike na kiume na wakati huo huo kuboresha mfumo wa mgao wa chakula ambao Iraq imeweka kwa familia zenye mahitaji na ustawi, ili hata watoto wanapojiunga na shule familia haziathiriki kutokana na watoto kutolewa kwenye mfumo huo.”

Hata hivyo WFP imeeleza kuwa utafiti ulifanywa kabla ya madhila ya hivi karibuni ya Mosul, na hivyo haugusii ukosefu wa chakula kwa watu waliofurushwa katika maeneo yenya machafuko.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo asilimia 2.5 ya watu wa Iraq wana uhaba wa chakula na hivyo msaada unahitajika haraka.