Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Umoja wa Mataifa walaani vikali mashambulizi ya makanisa nchini Misri

Umoja wa Mataifa walaani vikali mashambulizi ya makanisa nchini Misri

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amelaani vikali mashambulizi ya kigaidi yaliyotokea katika makanisa mawili ya dhehebu la Kikopitiki wakati wa ibada, na kukatili maisha ya watu 41 na kujeruhi zaidi ya mia moja katika miji ya Tanta na Alexandria nchini Misri hii leo.

Guterres ametuma salamu zake za rambirambi kwa familia za wahanga, serikali ya Misri na kuwatakia majeruhi afueni ya haraka, na anatumaini kuwa wahusika wa kitendo hiki cha kutisha watatambuliwa na kuletwa mbele ya sheria.

Wakati huo huo Baraza la Usalama pia limelaani vikali mashambulizi haya ya kinyama na imesema kwamba ugaidi wa aina yoyote ni tishio kubwa kwa amani na usalama ulimwenguni.

Kwa mantiki hiyo, wanachama wa baraza hilo wamesisitiza haja ya serikali husika kuleta watendaji, waandalizi, wafadhili na wadhamini wa vitendo ya kikagaidi mbele ya mkondo wa sheria kwa kulingana na majukumu yao chini ya sheria ya kimataifa,  pamoja na maazimio ya baraza hilo na limetoa wito wa kushirikiana kikamilifu na serikali ya Misri na mamlaka zingine husika katika kutatua suala hili.

Baraza pia limetuma salamu zake za rambirambi kwa familia za wahanga na kuwatakia majeruhi afueni.