Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto 27 wauawa kwenye shambulio la Idlib-UNICEF

Watoto 27 wauawa kwenye shambulio la Idlib-UNICEF

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF Alhamisi limethibitisha kwamba watoto 27 wamepoteza maisha kwenye shambulio la Idlib Syria Jumanne. Watu wengine 546 miongoni mwao watoto wengi wamejeruhiwa na idadi ya waliokufa inatarajiwa kuongezeka.

Mauji ya watoto Syria hayawezi kuendelea kuruhusiwa amesema mkurugenzi wa kikanda wa Syria Geert Cappelaere, akizitaka pande zote kwenye mzozo na walio na ushawishi katika vita hivyo kukomesha mara moja jinamizi hilo.

UNICEF na washirika wengine wanaendelea kusaidia waathirika wa shambulio hilo kwa kuwezesha kliniki tatu na hospitali nne ambazo zinatoa huduma ya kwanza, pia wanasaidia magari 9 ya kubeba wagonjwa ili kuwasafirisha hadi hospitali za jirani.

UNICEF pia inapeleka msaada muhimu wa vifaa vya afya na kushirikiana na wahudumu wa afya kuelimisha kuhusu huduma za afya za kukabiliana na mashambulizi ya kemikali.