Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ni marufuku na ni uhalifu kutumia silaha za kemikali:Baraza la usalama

Ni marufuku na ni uhalifu kutumia silaha za kemikali:Baraza la usalama

Wajumbe wa baraza la usalama Jumatano wamelaani vikali madai ya matumizi ya silaha za kemikali kwenye mji wa Khan Shaykhun nchini Syria Jumanne na kuelezea kusikitishwa kwao kwamba watu wanaendelea kuuawa na kujeruhiwa na na silaha hizo zilizopigwa marufuku na limejidhatiti kuhakikisha wahusika wakibainika kuwajibishwa.

Takribani watu 70 wameripotiwa kuuawa kwenye shambulio hilo na wengine zaidi ya 100 kujeruhiwa. Mwakilishi wa ngazi ya juu wa Umoja wa mataifa kuhusu masuala ya upokonyaji silaha Kim Won-Soo amewaarifu wajumbe wa baraza hatua zinazochukuliwa na shirika la kupinga matumizi ya silaha za kemikali OPCW kwamba uchunguzi bado unaendelea na kwamba amekuwa na mawasiliano na mkurugenzi wa shirika hilo ambaye

image
Mwakilishi wa ngazi ya juu wa Umoja wa mataifa kuhusu masuala ya upokonyaji silaha Kim Won-soo akiarifu baraza la usalama. Picha: UM/Rick Bajornas
(SAUTI YA KIM CUT)

“Amenijulisha kwamba ujumbe wa kusaka ukweli kuhusu silaha hizo wa OPCW unakusanya taarifa na kuzitathimini kutoka katika vyanzo mbalimbali vilivyopo na utapeleka timu mapema upatapo fursa. Endapo ikithibitishwa basi hilo litakuwa shambulio moja kubwa kabisa la silaha za kemikali Syria tangu la Ghouta mwahsriki mwa nchi Agost 2013.”

Balozi wa Marekani kwenye umoja wa Mataifa ambaye pia ni Rais wa baraza la usalama mwezi huu Nikki Haley akionyesha picha za waathirika wa shambulio hilo kwenye mjadala amesema baraza hilo ambalo ni mtetezi wa amani, usalama na haki za binadamu halitostahili kuvaa kofia hiyo endapo litashindwa kuchukua hatua kuzuia ukatili huo

image
Balozi wa Marekani kwenye umoja wa Mataifa ambaye pia ni Rais wa baraza la usalama mwezi huu Nikki Haley akionyesha picha za waathirika wa shambulio la kemikali akihutubia baraza la usalama. Picha: UM/Evan Schneider
(SAUTI YA NIKKI)

“Hatuwezi kufumbia macho picha hizo, hatuwezi kufumba akili zetu kuhusu kuchukua hatua. Hatujui kila kitu kuhusu shambulio la jana lakini kuna mengi ambayo tunajua. Tunajua shambulio la jana linabeba nembo ya matumizi ya silaha za kemikali ya uongozi wa Rais Assad, Tunajua uongozi wa Assad ulitumia silaha hizo dhidi ya watu wake siku za nyumatukio lililothibitishwa na timu ya uchunguzi ya baraza hili. Na tunajua shambulio la jana ni sheria mpya ya utawala wa kikatili wa Assad.”

Ameongeza kuwa wakati wa maneno matupu umekwisha sasa vitahitajika vitendo. Uingereza ambayo ni miongoni mwa wajumbe watano wa kudumu wa baraza la usalama kupitia balosi wake Matthew Rycrof imejutia uamuzi wa kura ya turufu wa mwezi Februari ambapo azimio lingepitishwa lingeweka vikwazo dhidi ya matumizi ya silaha za kemikali Syria.

image
Balozi wa Uingereza Matthew Rycrof. Picha: UM/Manuel Elias
(SAUTI YA RYCROFT)

“Tungeweza kutuma ujumbe ulio bayana siku ile, ishara ya wazi kwamba kutakuwa na madhara ya kutumia silaha hizo mbaya kabisa, kwa kukiuka sheria za kimataifa. Ujumbe wa wazi kwamba kuna mshikamano kwenye baraza la usalama, mshikamano wa kimataifa dhidi ya matumizi ya silaha hizi. Lakini baada ya Urusi na China kupiga kura ya turufu, inaonekana ujumbe pekee walioupeleka kwa Assad ni wa kumchagiza. Na jana tumeshuhudia athari za kura hizo za turufu.”

Balozi wa Urusi kwenye Umoja wa mataifa Vladmir Safrokov anasema king’ang’anizi cha kutaka kubadili utawala Syria ndio chachu ya zahma.

image
Balozi wa Urusi kwenye Umoja wa mataifa Vladmir Safrokov akihutubia baraza la usalama ya kujadili matumizi ya silaha za kemikali kwenye mji wa Khan Shaykhun nchini Syria Picha: UM/-Evan Schneider
(SAUTI YA SAFRONKOV CUT)

"Kila kitu kinaongozwa na haja ya mabadiliko ya serikali. Hiki king’ang’anizi cha kutaka mabadiliko ya serikali ndicho kinazuia kazi za Baraza la Usalama. Kwa hakika mnajaribu kuwa na Baraza la Usalama la kutoa bima ya uhalali wa mipango iliyo haramu. "

Hatimaye naibu balozi wa Syria kwenye Umoja wa Mataifa nchi iliyo katika kitovu cha mjadala wa leo Mounzer Mounzer hakufungwa kauli ya kulitetea taifa lake

image
Naibu balozi wa Syria kwenye Umoja wa Mataifa Mounzer Mounzer akihutubia baraza la usalama. Picha: UM/Evan Schneider
(MOUNZER CUT)

"Msimamo wa Serikali yangu kimsingi na kwa ukakamavu unakataa na kulaani uhalifu wa kutumia silaha za kemikali, au aina nyingine yoyote ya silaha za maangamizi, kwa mtu yeyote, popote, chini ya hali yoyote, na kwa sababu yoyote, na inachukulia kuwa ni uhalifu dhidi ya ubinadamu na ni kitendo kinachokataliwa kimaadili kitendo ambacho hakiwezi kuhalalishwa kwa hali yoyote ile"

Wajumbe wote 15 wa baraza la usalama walipewa fursa ya kuchangia mtazamo wao katika mjadala huo.