Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uganda sasa kufuatilia kesi za ICC kupitia simu za rununu

Uganda sasa kufuatilia kesi za ICC kupitia simu za rununu

Hatimaye huko Uganda, wahanga wa matukio ya uhalifu wa kivita yanayodaiwa kutekelezwa na Dominic Ongwen sasa wataweza kufuatilia mwenendo wa kesi hiyo kupitia simu ya rununu.

Hatua hiyo inafuatia mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa jinai, ICC kuzindua mfumo wa kupata ujumbe bila gharama kupitia simu za kiganjani na hivyo kuwezesha mwenendo wa kesi kufikia watu wengi zaidi licha ya kwamba iko The Hague, Uholanzi.

Msajili wa mahakama ya ICC Herman Von Hebel amesema kwa kufanya hivyo, wanahakikisha kuwa haki inatendeka na kwamba mtumiaji aliyejisajili anapata ujumbe kwa lugha za kiingereza, kiacholi na kiateso.

Mradi huo umewezeshwa kufuatia usaidizi wa shirika la Canada la Peace Geeks.

Dominic Ongwen mwenye umri wa miaka 70 anatuhumiwa kuhusika na uhalifu wa kivita kaskazini mwa Uganda kati ya mwaka 2000 na 2005 wakati akiwa kamanda wa waasi wa Lord's Resistanace Army LRA.