Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Azimio la IPU lataka hatua zaidi kukabili njaa kali Afrika na Yemen

Azimio la IPU lataka hatua zaidi kukabili njaa kali Afrika na Yemen

Mkutano wa 136 wa umoja wa mabunge duniani, IPU umepitisha azimio linalotaka hatua za dharura za kimataifa ili kuokoa mamilioni ya watu wanaokumbwa na njaa kali na ukame katika baadhi ya nchi za Afrika na huko Yemen.

Azimio hilo limepitishwa katika ajenda ya dharura wakati wa mkutano unaoendelea huko Dhaka, Bangladesh ambapo wabunge wameazimia kushinikiza serikali zao kutenga fedha kwa ajili ya kuepusha janga la kibinadamu.

Wamesema kwa mwaka wa tatu mfululizo wananchi kwenye maeneo hayo wanakabiliwa na njaa wakitaja Ethiopia na Kenya, miongoni mwa nchi 10 zenye idadi kubwa ya wakimbizi kuwa wakimbizi wako hatarini zaidi kuathiriwa na janga la njaa.

Azimio hilo la IPU limesisitiza kipaumbele cha ufadhili wa fedha kwenye huduma za kibinadamu na zilenge zaidi makundi kama vile watoto, wanawake na wazee.

Halikadhalika limesisitiza kuwa njaa kali kamwe isitumiwe kama silaha ya vita na wale watakaofanya hivyo wanapaswa kufikishwa mbele ya sheria.