Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Amani kwenye mabomu ya ardhini si amani ya kudumu- Guterres

Amani kwenye mabomu ya ardhini si amani ya kudumu- Guterres

Hakuna mtu yeyote anayepaswa kuishi kwa hofu pindi mapigano yanapomalizika, ni sentensi inayohitimisha ujumbe wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António  Guterres katika siku ya leo ya kimataifa  ya kutokomeza mabomu ya kutegwa ardhini.

Guterres anasema mabomu mengi ya kutengenezwa yanazidi kufichwa majumbani, shuleni na kutishia wananchi wakati huu ambapo mizozo inazidi kuongezeka na kuwa na uhusiano.

Hata hivyo amepongeza ofisi ya Umoja wa Mataifa inayosaidia kutokomeza mabomu hayo, UNMAS akisema kwa miaka 20 sasa imeleta nuru kwa wananchi ambao kwao ardhi yao sasa inaweza kutumika kwa manufaa baada ya mabomu kuteguliwa.

image
Mfanyakazi akiwa katika harakati za kutegua mabomu huko Goma, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, jukumu lililoongozwa na kituo cha Umoja wa Mataifa cha kuratibu kutegua mabomu, UNMACC. (Picha:UN /Sylvain Liechti)
Katibu Mkuu amesema amani bila kuteguliwa kwa mabomu si amani ya kudumu, hivyo ametoa wito kwa nchi wanachama kupatia kipaumbele suala hili pindi wanapojadili masuala ya amani na wanapotuma wafanyakazi wa misaada kwenye maeneo.

Amesema harakati za kutegua mabomu ni msingi wa kudumu wa kujikwamua na maendeleo.

Miongoni mwa mbinu ambazo UNMAS inatumia kuelimisha umma kuhusu hatari za mabomu ya kutegwa ardhini ni kupitia nyimbo ambapo katika kibao hiki wamemtumia mwanamuziki David Dube ambaye ni balozi mwema wa UNMAS nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC.

Balozi huyu mwema anaeleza kuwa mabomu hayo ya kutegwa ardhini hufanana na vitu mbali mbali kama vile vifaa vya kutumia majumbani.