Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kambi mbili za muda kutibu Fistula zafunguliwa Sudan Kusini

Kambi mbili za muda kutibu Fistula zafunguliwa Sudan Kusini

Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu, UNFPA ikishirikiana na Wizara ya Afya nchini Sudan Kusini leo wamefungua vituo viwili vya kutibu wanawake wenye ugonjwa wa Fistula ndani ya hospitali ya jimbo la Aweil na hospitali ya Juba Teaching kwenye mji mkuu wa Juba.

Shirika hilo limesema huduma hiyo ya bure itakayotolewa kwa muda wa wiki mbili itasaidia wanawake watakaosafirishwa kutoka maeneo mbalimbali kufanyiwa upasuaji wa marekebisho, na utafanywa na madaktari kutoka Nigeria na Ghana.

UNFPA imeongeza kuwa Fistula ni shimo katika njia ya uzazi ambayo husababishwa na uchungu wa muda mrefu na ukosefu wa matibabu wakati wa kujifungua, ugonjwa ambao humsababisha mwanamke kushindwa kudhibiti mkojo na mara nyingine husabisha kifo.