Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkutano wa usaidizi kwa Syria ukianza kesho, Lebanon yalalama

Mkutano wa usaidizi kwa Syria ukianza kesho, Lebanon yalalama

Mkutano wa kimataifa kuhusu usaidizi wa Syria ukianza kesho huko Brussels, Ubelgiji, Mwakilishi mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini Lebanon, Philippe Lazzarini ametoa wito kwa wadau kuongeza usaidizi wao wa kifedha kwa Lebanon ambayo inahaha kuhifadhi wakimbizi kutoka Syria.

Katika taarifa yake kuhusu mkutano huo unaofanyika wakati huu ambapo mgogoro wa Syria unaingia mwaka wa saba, Bwana Lazzarini amesema nchi hiyo inayohifadhi wakimbizi wa Syria zaidi ya milioni moja inakabiliwa na changamoto za kiuchumi na kiusalama.

Amesema Lebanon imetumia rasilimali zake kuliko uwezo wake na hakuna namna nchi hiyo inaweza kuendelea na usaidizi wake wakati hakuna dalili za kuisha kwa mgogoro.

Tangu kuanza kwa mgogoro huo mwaka 2011, kiasi cha dola bilioni 4.9 kimetolewa kwa ajili ya kuwahudumia wakimbizi nchini Lebanon kiasi ambacho hata hivyo hakitoshi kulingana na mahitaji.

Mkutano huo wa Brussels wa siku mbili, utahudhuriwa pia na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres.