Watu wenye usonji wanaweza kuleta mabadiliko: Guterres

3 Aprili 2017

Ikiwa watu wenye ugonjwa wa usonji watafurahia uamuzi na uhuru wao, watawezeshwa kuleta mabadiliko chanya katika mustakabali wetu wa pamoja, amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres.

Katika ujumbe wake wa kuadhimisha siku ya usonji duniani inayoadhimishwa April pili kila mwaka, Katibu Mkuu amesema ugonjwa huo ni tatizo la muda mrefu la mishipa ya fahamu linalojitokea wakati wa utoto na huchangiwa na kiwango cha uharibifu ya mitizamo ya tabia, mawasiliano na lugha ya kijamii.

Guterres amesema wakati baadhi ya watu wenye usonji wanaweza kuishi maisha ya uhuru, wengine wana ulemavu mkubwa na wanahitaji huduma na msaada wa muda mrefu katika maisha yao.

Ametaka watu kila mahali kutimiza wajibu wa kubadili mitizamo hasi dhidi ya watu wenye usonji huku akisema watu hao wana haki za kurithi kama watu wengine katika jamii, zikiwamo utambuzi sawa mbele ya sheria kwa mujibu wa mkataba wa Umoja wa Mataifa wa haki za watu wenye ulemavu.

Katika kuzipata haki hizo na uhuru wao wa kufanya uamuzi wao, na tuhakikishe wanapata mali na usaidizi kwa watu wenye usonji, amesema Guterres.

Ameongeza kuwa ikiwa watapatiwa usaidizi, kundi hilo litawezeshwa kukabiliana na hatua muhimu katika maisha , kama vile kuamua wapi na nani wa kuishi naye, kuoa au kuolewa na kuwa na familia, aina ya kazi ya kufanya, na usimamizi wa mapato binafsi.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter