Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wanamuziki wapazia kilio cha Yemen

Wanamuziki wapazia kilio cha Yemen

Nchini Yemen, mapigano yaliyoanza miaka miwili iliyopita, yamekuwa mwiba siyo tu kwa raia bali pia kwa wale wanaotumia nchi hiyo kama njia ya kupitia kuvuka ghuba ya Aden na bahari ya Sham kwenda nchi nyingine. Wakimbizi na wahamiaji wanakumbwa na majanga kama vile kutekwa, kutumikishwa na hata wengine kukosa chakula na huduma za msingi. Wengine wanakuwa wako safarini kwenda Ulaya lakini kupitia Yemen inakuwa ni pengine mwisho wa ndoto yao. Sasa kupitia uratibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR, wanamuziki sita kutoka Ethiopia, Misri na Somalia wameungana na kutunga kibao cha kuibua madhila wanayopata wakimbizi na wahamiaji hao huku wakihoji je sauti zao wakimbizi na wahamiaji hao zinasikika? Ungana basi na Assumpta Massoi aliyefuatilia kibao hicho kiitwacho Dangerous Crossing au kivuko cha hatari.