Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Makabila madogo Somalia yaomba serikali izuie ubaguzi

Makabila madogo Somalia yaomba serikali izuie ubaguzi

Ujumbe wa Muungano wa Afrika nchini Somalia, AMISOM pamoja na serikali ya Denmark, wamehitimisha mkutano wa ngazi ya juu wa siku tatu mjini Mogadishu, Somalia, uliojadili ujumuishaji na ukuzaji wa makabila madogo katika masuala ya nchi kwa lengo la kukuza amani na utulivu. Amina Hassan na ripoti kamili.

(Taarifa ya Amina)

AMISOM imesema mkutano huo umepitisha mpango rasimu wa kitaifa wenye lengo la kulinda haki za makabila hayo na kusitisha aina zozote za ubaguzi, mpango ambao pindi utakapokamilishwa utaingizwa katika mpango wa taifa wa maendeleo.

Baadhi ya mapendekezo kwenye mpango huo ni kubadili mfumo wa uchaguzi na upigaji kura, kuanzisha mfuko wa maendeleo wa makabila madogo , kuweka siku adhimu kwa ajili ya kuwatambua na kuwaheshimu kila mwaka, kuingiza historia na ustaarabu wa makundi haya katika mtaala pamoja na kuweka kando rasilimali za uwezeshaji wa kiuchumi.

Mkutano huo ambao AMISOM imebainisha kuwa uko ndani ya mamlaka yake ni sehemu ya kukuza amani na maridhiano na ni matumaini yake kwamba pindi yatakapowasilishwa bungeni, yatapitishwa na kutekelezwa.