Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mgogoro wa wakimbizi wahitaji wajibu wa pamoja-Hendricks

Mgogoro wa wakimbizi wahitaji wajibu wa pamoja-Hendricks

Balozi mwema wa heshima ya maisha wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR Barbara Hendricks ametoa wito kwa Muungano wa Ulaya kukumbuka maadili ya kuanzishwa kwake.

Akizungumza kwenye bunge la Muungano wa Ulaya kwenye maadhimisho ya miaka 60 ya mkataba wa Roma ametoa wito kwa nchi wanachama kutimiza wajibu wao katika kushughulikia changamoto ya kimataifa ya wakimbizi.

Wakati vita duniani vikisababisha mgogoro mkubwa wa kibinadamu na watu zaidi ya milioni 65 kutawanywa muimbaji huyo wa muziki wa classic mzaliwa wa Marekani amechukua fursa hiyo kumulika uzoefu wake wa zaidi ya miaka 30 na kurejelea wito wa haja ya wajibu wa pamoja kukabiliana na changamoto za sasa Ulaya.

Hendricks, ambaye ni balozi wa muda mrefu zaidi wa UNHCR ameonya dhidi ya kuruhusu wachuuzi wa hofu, chuki na kutengwa kupaza sauti juu na kufafanua kuhusu utambulisho wa taifa.

Hata hivyo, ameonyesha imani yake kwa nguvu ya pamoja ya muungano wa Ulaya ya kupambana na matatizo haya moja kwa moja, karibu miaka 25 baada ya kuchagua kushiriki katika kile alichokiita " ugumu huu, wenye utata na bado wa ajabu “.

Amewaomba wajumbe hao kuonyesha mshikamano na wakaimbizi kama ule ambao wangetaka uonyeshwe kwa familia zao endapo zingelazimika kukimbia.