Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ahadi ya kupatia makazi wakimbizi wa Syria yasuasua- UNHCR

Ahadi ya kupatia makazi wakimbizi wa Syria yasuasua- UNHCR

Wakati idadi ya watu wanaokimbia Syria ikivuka milioni 5 kutokana na vita vilivyodumu miaka sita, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR limetaka jamii ya kimataifa ichukue hatua zaidi kuwasaidia wapate hifadhi.

Kaminshna Mkuu wa UNHCR Filippo Grandi amesema bado kuna safari ndefu kupanua wigo wa makazi kwa wakimbizi hao wanawake, wanaume na watoto.

Akizungumza ikiwa ni mwaka mmoja tangu kufanyika kwa mkutano kuhusu Syria ulioahidi kuwapatia hifadhi wakimbizi 500,000 wa Syria ifikapo mwaka 2018, Bwana Grandi amesema hadi sasa ni nusu yao tu ndio wamefanikiwa.

Amesema iwapo jamii ya kimataifa inataka kufikia lengo iliyojiwekea mwaka jana, ni lazima hatua thabiti zichukuliwe mwaka huu.

UNHCR inakadiria kuwa takribani wakimbizi milioni 1.2 watahitaji makazi mwaka huu ambapo asilimia 40 kati yao ni raia wa Syria.