Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sudan Kusini yasifiwa kuondoa vizuizi barabarani

Sudan Kusini yasifiwa kuondoa vizuizi barabarani

Mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini, David Shearer, amepongeza mamlaka ya mji wa Gogrial, nchini humo kwa kuondoa vizuizi 7 kati ya 9 barabarani kuanzia mwezi Februari mwaka huu ili kurahisisha upitishaji wa misaada ya kibinadamu nchini humo. Taarifa zaidi na Amina Hassan.

(Taarifa ya Amina)

Bwana Shearer ambaye pia ni mkuu wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa Sudan Kusini, UNMISS, amesema mbali na kufikisha misaada, hatua hiyo pia italeta manufaa mengi kwa raia wa eneo hilo kama vile kufanya biashara bila vikwazo, kusafiri na ni mfano mzuri ambao umeigwa pia na miji jirani na anatarajia kuwa utasambaa katika majimbo mengine.

Ameongeza kuwa moja ya majukumu ya UNMISS nchini humo ni kulinda misafara ya kutoa misaada, akisema kwa kawaida msafara wa kilometa 1000 kutoka mji mkuu Juba hadi Bentiu utasimamishwa takriban mara 90, sawa na safari ya wiki mbili hadi tatu kulingana na hali barabarani, lakini kuchelewa huko mara nyingi husababishwa na muda ambao msafara huo unasimamishwa katika vizuizi hivyo.

Hivyo amesema kufikishwa kwa misaada bila ya vikwazo kutasaidia wakazi wa mji huo ambao sasa wamo hatarini kukosa chakula kutokana na mapigano na ukame.