Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNESCO yamtunuku mwandishi Dawit Isaak mzaliwa wa Eritrea

UNESCO yamtunuku mwandishi Dawit Isaak mzaliwa wa Eritrea

Dawit Isaak, mwandishi wa habari mzaliwa wa Eritrea mwenye uraia wa Sweden ambaye sasa yuko kifungoni, amechaguliwa na shirika la Umoja wa Mataifa la elimu sayansi na utamaduni UNESCO , kupokea tuzo ya kimataifa ya uhuru wa vyombo vya habari kwa mwaka 2017 ijulikanayo kama UNESCO/Guillermo Cano World Press Freedom Prize.

Bwana. Isaak alikamatwa katika msako wa vyombo vya habari uliofanyika Septemba 2001. Mara ya mwisho alisikika 2005, na wapi aliko sasa ni kitendawili kisicho na jibu.

Jopo huru la majaji wa kimataifa kutoka tasnia ya habari limempendekeza bwana Isaak kwa kutambua ujasiri wake, harakati zake na uwajibikaji wake katika kupigania uhuru wa kujieleza na pendekezo hilo limeidhinishwa na mkurugenzi mkuu wa UNESCO Irina Bokova.

Dawiti Isaak ambaye ni mawandishi wa habari, mtunzi wa riwaya na mwandishi wa vitabu alihamia Sweden mwaka 1987 na baadaye kuwa raia wa taifa hilo. Anaungana na orodha ya waandishi wengine wenye ujarisi ambao wamehakikisha jamii zao zinahabarishwa kwa kutumia kila njia. Tuzo hiyo inaambatana na fedha taslimi dola 25,000.