Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

David Beasley Mkurugenzi Mtendaji mpya wa WFP

David Beasley Mkurugenzi Mtendaji mpya wa WFP

Shirika la Mpango wa Chakula, WFP pamoja na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres wamemteua Bwana David Beasley wa Marekani kuwa mkurugenzi mtendaji wa shirika hilo, akichukua nafasi ya Etherine Cousin ambaye anamaliza muhula wake wa miaka mitano Aprili 4 mwaka huu.

Taarifa ya WFP imesema Bwana Beasley ambaye ni Mwenyekiti wa kituo cha mikakati ya kimataifa na alichaguliwa kuwa mwakilishi wa baraza la wawakilishi wa la Marekani akiwa na umri wa miaka 21, ni mwenye uzoefu na sifa kubwa itakayonufaisha shirika hilo.

Bi Cousin ambaye ameongoza shirika hilo katika wakati pekee uliokuwa na dharura kubwa na nyingi ulimwenguni amesema hata kabla ya uteuzi wake na katika mazungumzo naye, Bwana Beasley ana dhamira ya kufikia lengo la kutokomeza njaa la maendeleo endelevu, ameonyesha dhamira ya kuchagiza ongezeko la rasilimali katika shirika hilo ambalo hivi sasa linakumbwa na majanga manne makuu ya njaa.

Vile vile amesema amevutiwa na uelewa wake mkumbwa kuhusu shirika hilo na uelewa wa mpango wa kimkakati wa utekelezaji uliopitishwa na bodi ya uteuzi.