Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nyukilia itumike kwa maendeleo sio silaha-Tanzania

Nyukilia itumike kwa maendeleo sio silaha-Tanzania

Tanzania imesema inaunga mkono maendeleo ya teknolojia ya nyuklia katika kutibu magonjwa yasiyoambukiza kama vile saratani na utunzaji wa chakula dhidi ya uharibifu, lakini ikasisistiza kwamba matumizi ya silaha za nyukilia ni jinamizi kwa kila mmoja.

Hiyo ni sehemu ya tamko la serikali ya nchi hiyo katika mkutano uliofanyika hii leo katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York Marekani, uliolenga mazungumzo ya kuanzisha chombo cha kisheria cha kupiga marufuku silaha za nyuklia.

Akiwakilisha tamko hilo, Mwakilishi wa kudumu wa Tanzania katika ofisi ya Umoja wa Mataifa mjini New York Marekani, Balozi Modest Mero amesema teknolojia hiyo ina manufaa mengi na katika karne hii ugunduzi kama vile kutokomeza mbung’o, wadudu wanaoharibu matunda na hata kwa ajli ya kuendeleza nishati vimekuwa ni manufaa yakinifu.

Balozi Mero amesema nchi yake inatambua kuwa uangamizwaji wa nyukilia katika maghala ambapo makosa ya kibinadamu na ajali havikwepeki, ni ukumbusho kwamba ni tishio kwa binadamu.

Mataifa kadhaa yamewasilisha matamko yao katika mkutano huo kupinga matumizi ya nyukilia na kuunga mkono hoja ya uwepo wa chombo cha kisheria cha kupiga marufuku na kutowesha kabisa matumizi ya silaha za nyuklia katika mkutano huo wa siku tano ulioanza jana na unaotarajiwa kukakamilika Machi 31 mwaka huu.