Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Muda unayoyoma kwa watoto wanaokabiliwa na baa la njaa, ukame na vita

Muda unayoyoma kwa watoto wanaokabiliwa na baa la njaa, ukame na vita

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF limesema watoto hawawezi kusubiri, na dola milioni 255 zinahitajika haraka ili kukabiliana na mahitaji kaskazini mashariki mwa Nigeria, Somalia, Sudan Kusini na Yemen.

Mkurugenzi wa Mipango ya dharura wa UNICEF Manuel Fontaine amesema kutokana na funzo walilopata mwaka wa 2011 nchini Somalia ni kwamba muda waliotangaza baa la njaa , idadi isiyohesabika ya watoto tayari walishaaga dunia na hawawezi kukubali hali hiyo itokee tena.

(Sauti ya Christophe)

Watoto milioni 22 katika nchi hizi nne hawana chakula, ni wagonjwa, wamekimbia makwao na hawaendi shule na kati yao watoto milioni 1.4 wako katika hatarini ya kifo kwa ajili ya utapia mlo uliokithiri mwaka huu. Fedha hizo dola milioni 255 zitatusaidia kutoa chakula, maji safi, huduma za afya, elimu na ulinzi kwa miezi michache ijayo.

UNICEF imesema dola milioni moja kati ya fedha hizo zitasaidia mipango ya lishe, kuwachunguza watoto utapiamlo na kuwapatia chakula matibabu, na dola milioni 53 zitatengwa kwa huduma za afya ikiwa ni pamoja na chanjo.