Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tuna matumaini na mjadala wa kitaifa nchini Gabon - UM

Tuna matumaini na mjadala wa kitaifa nchini Gabon - UM

Wakati Gabon inajiandaa na mjadala wa kitaifa kesho Jumanne, Mwakilishi maalum wa Katibu mkuu wa umoja wa Mataifa kwa Afrika ya kati, UNOCA, Francois Louncény Fall amesema wana imani kubwa kuwa mjadala huo utaendeshwa kwa amani, utulivu na utakuwa jumuishi.

Taarifa ya UNOCA imesema kwa miezi miwili sasa Bwana Fall ameimarisha juhudi za kufanya majadiliano na wadau mbalimbali nchini Gabon ikiwa ni pamoja na viongozi wa serikali, upinzani, vyama vya kiraia, vijana na wanawake.

Kwa kuzingatia ajenda ya mjadala huo, Mkuu huyo wa UNOCA amesihi wadau wote kushiriki kwa nia njema ili kupanua fursa ya demokrasia na kuleta marekebisho yanayolenga kuimarisha utawala wa sheria na maridhiano ya kitaifa nchini Gabon.

Mjadala huo unafanyika kufuatia mzozo ulioibuka baada ya uchaguzi mkuu nchini Gabon na kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi wa rais mwezi Septemba mwaka jana.