Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNESCO yazindua kitabu cha mwongozo waandishi wa habari za ugaidi

UNESCO yazindua kitabu cha mwongozo waandishi wa habari za ugaidi

Shirika la Umoja wa mataifa la elimu sayansi na utamaduni UNESCO limezindua kitabu cha mwongozo kwa waandishi wa habari ili kuongeza uelewa wao zaidi katika kuandika habari kuhusu ugaidi.

Taarifa ya UNESCO imesema kitabu hicho kilichoandikwa na Jean-Paul Marthoz kitawezesha wanahabari kutekeleza majukumu yako ya kuhabarisha umma bila kuwapatia fursa magaidi ya kufanikisha lengo lao la kugawa wananchi.

Mathalani wawe makini ni nani wanamnukuu na ni ujumbe gani wanaotoa licha ya shinikizo kutoka kwa wasomaji, watazamaji na wasikilizaji.

Mifano ya hivi karibuni imetumika kuonyesha ni jinsi gani waandishi wa habari wanaweza kutoa taarifa juu ya waathirika wa ugaidi, kushughulikia uvumi, uchunguzi wa mamlaka, na kufanya mahojiano na magaidi.

Mwongozo huo wenye kurasa 110 unapatikana kwa lugha za Kiingereza na Kifaransa na unaonyesha changamoto za utoaji wa taarifa juu ya uwiano na hali tete kuhusiana na ugaidi.