Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Harakati za kutokomeza nyuklia zaanza, nchi 40 zasema hazitoshiriki

Harakati za kutokomeza nyuklia zaanza, nchi 40 zasema hazitoshiriki

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa leo limeanza awamu ya kwanza ya mkutano wake wa kujadili mbinu yenye nguvu kisheria ambayo itawezesha kutokomeza silaha za nyuklia ulimwenguni.

Akifungua mkutano huo, Mwenyekiti wa kikao hicho kitakachomalizika tarehe 31 mwezi huu, balozi Elayne Whyte Gomez wa Costa Rica amesema amani ni lazima iibuke mshindi dhidi ya silaha za nyuklia.

(Sauti ya Elayne)

“Tunapaswa kuongozwa kwa mashauriano na siyo kutokupatana. Tunapaswa kuongozwa na maafikiano na si uzembe.”

Katika mkutano huo, balozi Masud Bin Momen wa Bangladesh alisoma hotuba ya Rais wa Baraza Kuu Peter Thompson ambapo ameeleza kuwa lengo la kutokuwa na silaha za nyuklia bado halijafikiwa licha ya mkataba wa kutokomeza kutiwa saini zaidi ya miaka 70 iliyopita.

(Masoud cut) 

“Ingawa kiwango cha hifadhi ya silaha za nyuklia hivi sasa ni kidogo sana tangu kumalizika kwa vita baridi, bado ni dhahiri kuwa iwapo silaha za nyuklia zitaendelea uwepo, ni tishio lisilokubalika kwa usalama wa binadamu.”

Kabla ya kuanza kwa kikao hicho wawakilishi wa Ufaransa, Marekani na Uingereza kwenye Umoja wa Mataifa walizungumza na wanahabari na kueleza kuwa nchi hizo tatu na nyingine 37 hazitashiriki mkutano huo unaolenga kutokomeza kabisa nyuklia kwa maelezo kuwa hatua hiyo haitazaa matunda yoyote.