Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sudan yafungua njia salama kukabili njaa Sudan Kusini

Sudan yafungua njia salama kukabili njaa Sudan Kusini

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Misaada ya Kibindamu, OCHA imekaribisha hatua ya serikali ya Sudan ya kufungua njia mpya na salama kwa ajili ya kupitisha misaada ya kibinadamu, hatua ambayo itaokoa maisha ya watu 100,000 wanaokumbwa na njaa kali nchini Sudan Kusini.

Barabara hiyo ya urefu wa kilometa 500 yenye kuanzia El Obeid katikati mwa Sudan hadi Bentiu, Sudan Kusini itawezesha Shirika la mpango wa chakula duniani, WFP kufikisha tani 11,000 ya chakula wiki hii, kiasi ambacho kitatosheleza lishe ya miezi mitatu kwa watu 300,000 nchini humo.

Shirika hilo limesema hatua hiyo ni muhimu wakati huu kabla mvua hazijaanza mwezi Mei na inadhihirisha ushirikiano wa Sudan na nchi hiyo pamoja na jumuiya ya kimataifa katika kuzuia janga la njaa ambalo linaweza kuathiri watu wengine milioni moja.