Licha ya juhudi za kimataifa , milio ya risasi na mabomu yaendelea kunguruma Yemen:O’Brien

27 Machi 2017

Licha ya juhudi za kimataifa za kuleta suluhu ya kudumu ya kisasa Yemen, milio ya makombora, mabomu, risasi na vifaru sasa imekuwa ada katika maisha ya kila siku nchini humo.

Hayo yamesema na Stephen O’Brien msaidizi wa Katibu mkuu katika masuala ya kibinadamu na misaada ya dharura, katika taarifa yake kuhusu miaka miwili baada ya kuzuka machafuko Yemen.

Amesema maelfu ya raia wameuawa, wakiwemo wasichana na wavulana zaidi ya 1400, wengi wa watoto hao walitoka majumbani kwao kuelekea shuleni na hawakurejea tena, huku raia wengine kwa maelfu wakijeruhiwa.

Ameongeza kuwa vita, kutokuwepo usalama na mbinu zinazotumia na pande kinzani vimesambaratisha uchumi wa Yemen na kuongeza tatizo la uhaba wa chakula, watu milioni 3 kukimbia makwao na kuathri kazi za wahudumu wa misaada ambao lengo lao ni kupunguza madhila na kuokoa maisha.

O’Brien amesema leo hii zaidi ya Wayemini milioni 19 ikiwa ni zaidi ya theluthi mbili ya watu wote wanahitaji msaada wa kibinadamu na milioni saba kati yao wanakabiliwa na njaa.

Kikubwa zaidi amesema watu wa Yemen wamechoka na wanataka pande kinzani kujikita katika majadiliano ya kisiasa au mtafaruku huu uliosababishwa na binadamu hautokwisha.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter