Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ushirika imara ni muhimu kwa suluhu endelevu ya wakimbizi Ugiriki:UNHCR

Ushirika imara ni muhimu kwa suluhu endelevu ya wakimbizi Ugiriki:UNHCR

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR, Jumatatu limesema juhudi za pamoja na kuimarisha ushirikiano ni muhimu sana katika kuboresha hali kwa waomba hifadhi na wakimbizi nchini Ugiriki na limetoa mapendekezo manane ya kusaidia kuhakikisha msaada endelevu kwa wakimbizi nchini humo.

Kamishina mkuu wa wakimbizi Filipo Grand amesema , UNHCR inajihusisha kikamilifu kutafuta suluhu ya kudumu nchini Ugiriki pamoja na serikali za Muungano wa Ulaya, pia ameongeza kuwa hali ya Ugiriki inaweza kudhibitiwa, inachohitaji ni kutoka katika hali sasa ya dharura kuingia katika mfumo endelevu ambao waomba hifadhi na wakimbizi wanapata huduma za msingi.

Mengine aliyotaja ni kutoa kipaumbele katika kuboresha hali ya mapokezi wanakowasili wahamiaji na wakimbizi akisema hilo litasaidia kuzuia na kupambana na unyanyasaji wa kingono na ukatili wa kijinsia ambao unawakabili waomba hifadhi wengi hususani wanawake na watoto.