Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Vita vikiingia mwaka wa pili familia Yemen zageukia hatua kujikimu: UNICEF

Vita vikiingia mwaka wa pili familia Yemen zageukia hatua kujikimu: UNICEF

Baada ya miaka miwili ya vita, familia nchini Yemen zinageukia hatua kali ili kukidhi mhitaji ya watoto wao, limesema shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF katika ripoti yake iliyotolewa Jumatatu.

Ripoti inasema njia za kujikimu zimesambaratishwa na machafuko na kuigeuza Yemen kuwa moja ya nchi zenye tatizo kubwa la uhakika wa chakula na dharura ya utapia mlo duniani.

Familia sasa zina haha kupata mlo, zikila kidogo, vyakula visivyo na lishe ya kutosha au kuruka mlo kabisa. Kwa mujibu wa UNICEF karibu nusu milioni ya watoto wana utapia mlo uliokithiri, ikiwa ni ongezeko la asilimia 200 tangu mwaka 2014 na hivyo kuongeza hatari ya baa la njaa.

Kwa mujibu wa ripoti karibu asilimia 80 ya familia Yemen ziko katika madeni na nusu ya watu wote wanaishi kwa chini ya dola mbili kwa siku.

Rasilimali katika familia zinapungua na watoto zaidi wanaingizwa vitani na pande kinzani na wengine kushinikizwa katika ndoa za mapema.

Hivi sasa zaidi ya theluthi mbili ya wasichana wanaolewa kabla ya kutimiza miaka 18 , ikilinganishwa na asilimia 50 kabla ya vita.