Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

OCHA yalaani vikali mauaji ya wahudumu sita wa misaada Sudan Kusini:

OCHA yalaani vikali mauaji ya wahudumu sita wa misaada Sudan Kusini:

Mratibu wa masuala ya kibinadamu wa shirika la Umoja wa Mataifa OCHA nchini Sudan Kusini Eugene Owusu, amelaani vikali mauaji ya wafanyakazi sita wa misaada yaliyofanyika Jumamosi Machi 25 wakiwa safarini kutoka Juba kuelekea Pibor.

Katika taarifa yake Bwana Eugen Owusu amesema amesikitishwa na kughadhibishwa na mauaji hayo ya kinyama , katika wakati ambao mahitaji ya kibinadamu yamefikia kiwango kikubwa na kuongeza kuwa ni kitendo kisichokubalika, watu wanaojaribu kusaidia wanashambuliwa na kuuawa.

Shambulio hilo linalowakilisha idadi kubwa ya mauaji ya wahudumu wa misaada katika wakati mmoja tangu kuanza kwa machafuko Sudan Kusini limefanyika baada ya mashambulio mingine mawili dhidi ya wahudumu wa misaada mwezi huu.

Bwana Owusu amesema tarehe 14 Machi msafara wa misaada ulishambuiliwa huko Yirol Mashariki na mhudumu mmoja wa afya na mgonjwa waliuawa, na tarehe 10 Machi mfanyakazi wa NGO alitekwa mjini Mayendit na kundi la watu wenye silaha na kuachiliwa siku nne baadaye.

Wahudumu wa misaada takribani 80 wameuawa tangu kuanza kwa mgogoro wa Sudan Kusini Desemba 2013 na 12 wameuawa 2017 pekee.