Sudan Kusini ichunguze na kushikilia wauaji wa wahudumu wa misaada:UNMISS

Sudan Kusini ichunguze na kushikilia wauaji wa wahudumu wa misaada:UNMISS

Mwakilishi maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini , David Shearer ameitaka serikali ya Sudan Kusini kuchunguza na kuwashilikilia wauaji wa wahudumu sita wa misaada ya kibinadamu.

Wafanyakazi hao kutoka shirika la kitaifa lisilo la kiserikali waliripotiwa kushambuliwa katika gari lao kwenye eneo linalodhibitiwa na serikali katika barabara ya Upper Juba-Pibor Jumamosi asubuhi.

Miili yao ilikutwa barabarani na wafanyakazi wengine wa misaada waliokuwa nyumba katika msafara mmoja. Bwana Shearer amesema Umoja wa Mataifa unalaani vikali shambulio hilo la kikatili lililopoteza maisha ya watu bure na kwamba mauaji hayo ya kinyama

image
Mtu mwenye silaha mjini Pibor, jimbo laJonglei Sudan Kusini. Pibor imeshuhudia machafuko ambayo yamesababisha maelfu kukimbia, na uharibifu mkubwa wa mali na maisha. Picha na OCHA/Cecilia Attefor
(SAUTI DAVID SHEARER)

"Ni ya kukemewa kabisa, kwa sababu wafanyakazi hawa wa misaada walikuwa wakijitolea kupunguza madhila yanayoendelea wa watu wa Sudan Kusini.Na serikali inahitaji kuchunguza na kuwashikilia wahusika, wasiruhusiwe kutowajibishwa, kusiwe na ukwepaji sheria linapokuja suala la mauaji ya wahudumu wa misaada. Pia kunahitajika kuwa na usitishaji uhasama haraka na mazungumzo ya amani kuanza upya la sivyo nchi itaendelea kumeguka na kusababisha machafuko zaidi na hususani dhidi ya watu ambao wako hapa kuwasaidia raia wa Sudan Kusini. ”

Pia ametuma salamu za rambirambi kwa familia , jamaa na wafanyazi wa wahudumu hao waliopoteza maisha . Vifo vyao vimefanya idadi ya wahudumu wa misaada waliouawa Sudan Kusini tangu mwaka 2013 kufikia 80, ikiwa ni ishara kwamba Sudan Kusini ni moja ya nchi hatari zaidi duniani kuwa muhudumu wa misaada.