Skip to main content

Machafuko mapya Damascus na kwingineko yatia hofu: De Mistura

Machafuko mapya Damascus na kwingineko yatia hofu: De Mistura

[caption id="attachment_313488" align="aligncenter" width="620"]demistura

Mwakilishi maalumu wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Syria, Staffan de Mistura, amesema anatiwa hofu na mapigano ya karibuni Damascus, Hama na kwingineko Syria.

Amesema ukiukwaji unaoongezeka hivi karibuni unatishia mustakhbali wa amani uliojadiliwa kupitia mikutano ya Astana, ukiwa na athari mbaya kwa usalama wa raia wa Syria , fursa za misaada ya kibinadamu na kasi ya mchakato wa kisiasa.

Kwa mantiki hiyo amewatumia barua mawaziri wa mambo ya nje wa Iran, Urusi na Uturuki ambao ni wadhamini wa mkataba wa usitishaji uhasama wa Syria ulioanza kutekelezwa Desemba 30 mwaka 2016.

Amewaomba kuchukua hatua haraka za kuhakikisha usitishaji mapigano unaendelea , pia ameelekeza wito huo kwa mataifa ya Urusi na Marekani kama wenyeviti wenza wa kundi la kimataifa la msaada kwa Syria, ISG.

Bwana de Mistura amekumbusha kwamba juhudi za pamoja za Iran, Urusi na Uturuki za kuhakikisha usitishaji uhasama hazina mjadala kwamba zitaimarisha mazingira Syria na kuchangia hali bora kwa ajili yakupiga hatua katika mchakato wa kisiasa.