Ni saa moja ya kujali mazingira duniani:Guterres
Kwa mara ya Kumi, leo Jumamosi jioni, watu kila mahali watashiriki katika “saa moja ya kujali mazingira ulimwenguni” kama ishara ya kuchukua hatua dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.
Katika ujumbe wake kuhusu tukio hilo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema mabadiliko ya tabianchi yanaendelea kuhatarisha maisha na vipato duniani kote.
Mwaka jana ilikuwa tena mwaka uliovunja rekodi ya juu zaidi ya joto. Ameongeza kuwa Mkataba wa Paris unatupa fursa ya kipekee ya kuzuia kupanda kwa kiwango cha kimataifa cha joto, kukuza nishati safi kwa wote na kujenga mustakabali endelevu.
Ametoa wito kwa serikali na sekta binafsi ni lazima ziongeze juhudi zaidi. Hivyo pia watu binafsi. Amesema ili Kuijenga kesho iliyo endelevu, inamtegemea kila mmoja wetu leo.
Ameitaka dunia kuungana naye katika kuzima taa zao Machi 25 saa 8:30 usiku.
Akisema kutoka kwenye giza, tunaweza kujenga dunia endelevu na yenye umoja kwa wote.