Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wakati baadhi ya mifumo ya utumwa imetokomezwa mipya inaibuka-Guterres

Wakati baadhi ya mifumo ya utumwa imetokomezwa mipya inaibuka-Guterres

Wakati baadhi ya mifumo ya utumiwa ikiwa imetokomezwa mingine inaibuka na kuleta athari kubwa duniani ikiwemo usafirishaji haramu wa binadamu na kazi za shuruti, na hivyo kukumbusha kwamba tuliyojifunza jana inamaanisha kuyatumia kukabili madhila ya leo.

Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres katika hafla maalumu ya kumbukizi ya kuwaenzi waathirika wa biashara ya utumwa na biashara ya utumwa ya Atlantiki iliyofanyika kwenye baraza kuu la Umoja wa Mataifa Ijumaa

Ameongeza kuwa dunia isiufunge kabisa ukurasa huo wa kiza katika historia ya binadamu, na ni lazima daima kukumbuka mchango wa nchi nyingi katika biashara hiyo ikiwepo Ureno iliyokuwa kinara wa wafanfakazi wahamiaji wa shuruti na kuwapora mamilioni ya watu utu wao na mara nyingi maisha yao. Amesema vidonda vya enzi hizo vinatoneshwa tena

(SAUTI YA GUTERRES )

“Urithi wa utumwa unasikika zama hizi. Dunia bado haijautokomeza ubaguzi wa rangi. Nchi nyingi bado wanakabiliwa na mifumo ya kiuchumi na maamuzi yaliyowekwa muda mrefu uliopita. Familia nyingi bado wanahisi kiwewe kilichowekwa katika enzi za mababu zao. Ni lazima tuendelee kutambua maumivu ya kudumu ya urithi huu hata katika wakati wa sasa”.

Ameongeza kuwa kauli mbiu yam waka huu ni “kutambua urithi na mchango wa watu wa asili ya afrika “ ikitualika kuenzi mafanikio ya Waafrika walio ughaibuni.

(SAUTI YA GUTERRES)

“Tunauona mchango huo katika kila nyanja ya mafanikio ya binadamu. Vizazi vya watumwa vimeweka historia katika ubunifu, wachumi na wanasheria, pia kama waandishi na wanazuoni, wasanii na wanamichezo na pia kama wanasiasa na viongozi wa haki za kiraia.”

Ametoa wito kwa dunia katika wakati huu wa mgawanyiko mkubwa kuungana dhidi ya chuki na kujenga ulimwengu huru na wenye kuthamini utu kwa wote.