Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wakimbizi wa ndani Gambella Ethiopia wanufaika na msaada: IOM

Wakimbizi wa ndani Gambella Ethiopia wanufaika na msaada: IOM

Wakimbizi wa ndani 332 walio kwenye mazingira magumu wamenufaika na msaada kutoka shirika la kimataifa la uhamiaji, IOM nchini Ethiopia ikishirikiana na Ofisi inayoshughulikia maafa na uhakika wa chakula katika mkoa wa Gambella DPFSA. Msaada huo ulikuwa wa vifaa muhimu na kusaidia kaya, fedha ili kukidhi mahitaji yao ya msingi.

Taarifa ya IOM imesema kuwa mashambulizi ya hivi karibuni baina ya makabila katika maeneo ya mpakani wa Ethiopia mkoa wa Gambella yamesababisha familia zilizoathirika kukimbia makazi yao zikieleza kuwa vijiji vyao vilishambuliwa na wahusika ambao waliiba ng'ombe, kuteka watoto na kuchoma nyumba zao moto.

Mkuu wa ofisi ya IOM mkoani humo Miriam Mutalu, amesema watu walikimbia ghasia bila chochote na wana hofu kubwa ya kurejea katika vijiji vyao. Bado wako hatarini na wanahitaji haraka msaada wa kibinadamu.

IOM imesema mpango huu wa majaribio wa kutoa fedha na vocha ni sehemu ya usambazaji uliofanywa Machi 13-14 na kushirikisha masoko yaliyopo, na hivyo basi kuchangia katika uchumi wa jamii. Waathirika hao walisaidiwa vocha ya kupata vifaa 15 visivyo chakula ikiwa ni pamoja na vibuyu, vyombo vya kupikia, sabuni pamoja na vifaa vingine. IOM pia ilitoa vyandarua na dola 52 taslimu kwa kila kaya na kwa kila familia ili kutumia kununua mahitaji ya ziada.