Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Japo kuna changamoto, ulinzi wa amani umeokoa maisha- Ladsous

Japo kuna changamoto, ulinzi wa amani umeokoa maisha- Ladsous

Baada ya miaka sita ya kuhudumu kama Mkuu wa operesheni za ulinzi wa amani za Umoja wa Mataifa, Hervé Ladsous anahitimisha jukumu hilo akisema ingawa kulikuwa na changamoto bado wamepata mafanikio ikiwemo kuokoa raia.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini New York, Marekani kabla ya kumaliza mkataba wake tarehe 31 mwezi huu, Bwana Ladsous ametaja mafanikio kuwa ni pamoja na ulinzi wa raia kwenye mapigano akitolea mfano Sudan Kusini.

(Sauti ya Ladsous)

“Ndio naweza kukiri kuwa kuna wakati kulikuwa na makosa, na kila kosa ni kosa moja kwa wengi, lakini wakati huo huo, ni watu wangapi tumeokoa hata huko Juba?. Nimetembelea kituo cha kuhifadhi raia, wasudan kusini 220,000 sasa wanahifadhiwa, na penginepo wasingalikuwa hai kama tusingewapeleka kwenye kituo chetu. Lakini kuna matarajio makubwa na hivyo ni lazima tujaribu kwa kadri ya uwezo wetu kukidhi viwango.”

Alipoulizwa na waandishi wa habari kuhusu kitendo cha Baraza la Usalama kupinga mapendekezo ya sekretarieti ikiwemo vikwazo dhidi ya Sudan Kusini, Bwana Ladsous amesema ni kweli baadhi ya nchi zinapinga lakini ..

(Sauti ya Ladsous)

“ Bado nasisitiza kuwa vikwazo vya silaha kwa pande zote za mzozo wa Sudan Kusini, siyo tu serikali, ingekuwa na maana sana. Nchi hiyo sasa ni magofu.”

Alipoulizwa kuhusu mwelekeo wa Marekani kupunguza bajeti yake kwa Umoja wa Mataifa na kutoa asilimia 25 tu ya kiwango inachotoa sasa, Bwana Ladsous amesema..

(Sauti ya Ladsous)

“Tunaishi na kile tunachopatiwa na vyombo vya Umoja wa Mataifa na tunapanga mipango yetu kwa mujibu kile ambacho tunapatiwa.”

Nafasi ya Bwana Ladsous inachukuliwa na Jean-Pierre Lacroix, ambaye naye pia anatoka Ufaransa.